Uga sumaku wa Dunia
From Wikipedia, the free encyclopedia
Uga sumaku wa Dunia (kwa Kiingereza: geomagnetic field, Earth's magnetic field) ni uga sumaku ambao unazunguka Dunia. Unaenea kuanzia kiini cha Dunia hadi anga-nje unapoathiriana na upepo wa Jua (mkondo wa chembe zenye chaji kutoka Jua). Ugasumaku wa Dunia unakinga uhai duniani dhidi ya mnururisho haribifu kutoka anga-nje
Uga sumaku wa Dunia unaundwa na mzunguko wa Dunia; mzunguko huo unasababisha mikondo ya umeme kutokea kwenye kiini cha Dunia ambako joto la ndani linatoka nje.[1] Uga sumaku huo si wa kudumu ukijulikana umeshabadilika mara kadhaa katika historia ya Dunia.[2]
Uga sumaku wa Dunia huwa na ncha sumaku zinazopatikana karibu na ncha za kijiografia za Dunia. Ncha sumaku huhama mara kwa mara; kwenye mwaka 2007 ncha sumaku ya kaskazini ilikuwa na umbali wa km 960 kutoka ncha ya kijiografia ikiendelea kuhama takriban kilomita 50 kila mwaka[3]. Dira hutumia uga sumaku huo kudokeza nchani, lakini ilhali kuna tofauti kati ya ncha sumaku ya kaskazini na ncha ya kijiografia ya kaskazini ni lazima kujua tofauti hiyo kwa mwongozo wa safari za meli au ndege.