Terakota
From Wikipedia, the free encyclopedia
Terakota ni sanaa na vifaa vya ufinyanzi vinavyotengenezwa kwa kutumia udongo mwekundu unaochomwa, mara nyingi bila ganda la kioo usoni mwake. [1] [2] [3] [4] [5]
Jina limetokana na neno la Kiitalia terracotta ("udongo uliochomwa"). Kimsingi hakuna tofauti kubwa kati ya matofali ya kuchomwa na terakota, ila kazi za terakota ni lazima kutekelezwa kwa umakini zaidi na kuchagua vema udongo unaofaa.
Mifano ya kazi za terakota ni pamoja na sanamu, vyombo vya mapambo, picha kwenye uso wa vyombo, pia sura ya mapambo ya nyumba, lakini pia vifaa sahili kama mabomba ya ufinyanzi kwa ajili ya maji.
Mifano mashuhuri sana ni sanamu za tamaduni za kale zilizodumu miaka elfu kadhaa kwa sababu udongo wa ufinyanzi, kama uliteuliwa vema na kuchomwa vema, utadumu karne nyingi. Kati ya mifano mashuhuri ni sanamu za "Jeshi la Terakota" pale China, sanamu za Nok na terakota za Ugiriki ya kale.
Rangi ya vifaa visivyotiwa ganda la kioo mara nyingi ni nyekundu-kahawia; kuna pia mifano ya njano inayotumia udongo tofauti.
Terakota inapokea rangi lakini haiwezi kung'aa hadi kuchomwa mara ya pili ambako uso wa nje hufunikwa na tabaka la kioo.