Nabii Zekaria
From Wikipedia, the free encyclopedia
Zekaria (kwa Kiebrania זְכַרְיָה, Zekaria, "YHWH amekumbuka"; kwa Kigiriki Ζαχαρίας, Zakharias; kwa Kilatini Zacharias; kwa Kiarabu زكريا Zakariya au Zakkariya) alikuwa nabii wa Mungu mjini Yerusalemu kati ya mwaka 520 KK na 518 KK[1].
Habari zake zinapatikana hasa katika kitabu chake, cha 11 kati ya vile 12 vya Manabii Wadogo katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na kwa hiyo pia katika Agano la Kale la Biblia ya Kikristo.
Humo (Zek 1:1) anajitambulisha kama "mwana wa Berakia, mwana wa Iddo", ingawa kitabu cha Ezra (Ezra 5:1 na 6:14) kinamuita tu "mwana wa Iddo".
Kazi ya nabii huyo, iliyoanza wakati uleule alipotabiri nabii Hagai, ni mwanzo wa kipindi cha mwisho cha unabii katika Israeli kabla ya ujio wa Yohane Mbatizaji na Yesu Kristo.
Tofauti na Hagai, Zekaria hakuishia upande wa ujenzi mpya wa hekalu la Yerusalemu, bali alisisitiza pia utakaso wa waamini na ibada zao.
Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu.
Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 6 Septemba[2] lakini pia 8 Februari na 31 Julai.