Karl Barth
From Wikipedia, the free encyclopedia
Karl Barth (tamka bart; 10 Mei 1886 - 10 Desemba 1968) alikuwa mwanatheolojia wa Ukristo wa kireformed kutoka nchini Uswisi. Barth anajulikana zaidi kwa ufafanuzi wake wa Waraka kwa Warumi, kwa nafasi yake katika Kanisa la Ungamo huko Ujerumani wakati wa utawala wa Adolf Hitler, kwa utungaji wa Azimio la Barmen [1] [2] na hasa kwa muhtasari wake mkubwa wa Elimu ya Imani ya Kanisa (Church Dogmatics, Kirchliche Dogmatik) [3] iliyochapishwa kwa juzuu nyingi kati ya miaka 1932-1967. [4] [5]
Sawa na wanatheolojia wengi wa Kiprotestanti wa kizazi chake, Barth alielimishwa katika teolojia ya kiliberali iliyoathiriwa na Adolf von Harnack, Friedrich Schleiermacher na wengine. [6] Baada ya masomo, alianza kazi yake ya uchungaji katika kijiji cha Safenwil ambako wakazi wengi walifanya kazi viwandani; huko alijulikana kama "Mchungaji Mwekundu wa Safenwil" [7] na alizidi kukatishwa tamaa na Ukristo wa kiliberali ambao alikuwa amefundishwa ndani yake. Hii ilimfanya aandike toleo la kwanza la kitabu chake Waraka kwa Warumi (aka Warumi I), kilichochapishwa mwaka wa 1919, ambamo aliazimia kusoma Agano Jipya kwa njia tofauti.
Barth alianza kujulikana kimataifa tangu kuchapishwa mnamo 1921 chapa ya pili ya ufafanuzi wake, Waraka kwa Warumi, ambamo alijitenga na theolojia ya kiliberali waziwazi. [8]
Aliwashawishi wanatheolojia wengi muhimu kama vile Dietrich Bonhoeffer ambaye aliunga mkono Kanisa la Ungamo, na Jürgen Moltmann, Helmut Gollwitzer, James H. Cone, Wolfhart Pannenberg, Rudolf Bultmann, Thomas F. Torrance, Hans Küng, na pia Reinhold Niebuhr na Jacques Ellul pamoja na waandishi wa riwaya kama vile Flannery O'Connor, John Updike, na Miklós Szentkuthy.
Barth pia alikuwa na ushawishi mkubwa juu ya maadili ya Kikristo ya kisasa, [9] [10] akiathiri kazi ya wanamaadili kama vile Stanley Hauerwas, John Howard Yoder, Jacques Ellul na Oliver O'Donovan. [9] [11]