Anania wa Damasko
From Wikipedia, the free encyclopedia
Anania wa Damasko (jina kwa Kigiriki ni Ἀνανίας, kutokana na Kiebrania חנניה, Hananiah, yaani, "Aliyefadhiliwa na Bwana"[1]) alikuwa Myahudi wa karne ya 1 anayejulikana katika kitabu cha Matendo ya Mitume (9:10-19 na 22:12-16).
Humo tunasikia kwamba alikuwa mwanafunzi wa Yesu na kwamba, akiwa Damasko (Siria), alikuwa na sifa ya "mtu wa ibada kadiri ya sheria, aliyeheshimiwa na Wayahudi wote" (Mdo 22:12)[2].
Miaka 6 hivi baada ya kufufuka, alitokewa naye na kuagizwa kwenda kwa Saulo wa Tarso, nyumbani mwa Yuda kwenye Njia Nyofu, ili kumponya upofu na kumuelimisha katika dini mpya iliyoitwa baadaye Ukristo.
Alipopata agizo hilo, Anania alisita kwa kuwa alimuogopa Saulo kutokana na juhudi zake dhidi ya Wakristo, lakini Yesu alisisitiza aende, akieleza kwamba mtu huyo ni "chombo kiteule kwake, ili kufikisha jina lake kwa mataifa, kwa wafalme na kwa wana wa Israeli". (Mdo 9:15).
Anania alipotii, alimwekea Saulo mikono kichwani na kufanya magamba ya machoni mwake yadondoke. Kisha kumuelimisha kidogo, alimbatiza nyumbani humo (Mdo 9:18; 22:16).
Baada ya tukio hilo, hakuna habari za hakika juu ya Anania. Kadiri ya mapokeo, Anania alifia dini huko Eleutheropolis.[3]
Anaheshimiwa kama mtakatifu tarehe ya sikukuu ya Wongofu wa Mtume Paulo, 25 Januari[4].