Mkunjo (jiolojia)
From Wikipedia, the free encyclopedia
Mkunjo (kwa Kiingereza: fold) kwa maana ya jiolojia unatokea pale ambako tabaka la mwamba lililokaa kibapa linaathiriwa na miendo katika ganda la Dunia na kupindwa kutokana na shinikizo na jotoridi kubwa. Kwa kawaida sababu ni miendo ya gandunia yaani pale ambako mabamba (vipande vya ganda la Dunia) husukumana.
Mikunjo hutokea mara nyingi katika matabaka ya mwamba mashapo lakini inatokea pia katika miamba ya volkeno.
Kiwango cha kukunjwa hutofautiana kwa ukubwa kuanzia mikunjo midogo sana inayotambuliwa katika hadubini tu, hadi kutokea kwa safu za milima zinazoweza kuitwa milima kunjamano kama vile Himalaya, Alpi, Andes au Rocky Mountains.