Hija
From Wikipedia, the free encyclopedia
Hija (kutoka Kiarabu حج, hajj, kitenzi kuhiji) ni ziara ya kidini yaani ni safari inayofanyika kwa sababu ya dini, ikilenga patakatifu fulani.
Kwa maana ya kiroho, maisha yote ni safari ya kumuelekea Mungu au uzima wa milele n.k.
Sababu ya kwenda mahali maalumu ni tumaini la kuwa karibu zaidi na imani mahali ambako mambo muhimu ya historia ya dini husika yalitokea; mara nyingi pia imani ya kwamba sala itakuwa na nguvu au mafanikio zaidi pale.
Desturi ya kuhiji iko katika dini mbalimbali.
- Wahindu huhiji mahali pengi hasa mji wa Benares na mto Ganges.
- Uyahudi tangu zamani unatia maanani hasa hija ya kwenda Yerusalemu, iliyokuwa ya lazima katika sikukuu mbalimbali kwa waumini kuanzia umri wa kubalehe; unaendelea hata baada ya hekalu la mji huo kubomolewa kabisa mwaka 70 BK.
- Wakristo hasa wa madhehebu ya Kiorthodoksi na Katoliki wanajua hija kwenda Yerusalemu, Roma na mahali pengine.
- Waislamu huwa na hajj kutembelea Makka, Washia wanatembela pia makaburi ya maimamu wao huko Najaf, Karbala, Mashhad na penginepo. Mwislamu aliyetimiza safari hii anapokea cheo cha "alhaji" kama sehemu ya jina lake.